Vidokezo vya Ujasiriamali

Mradi

Katika shughuli za kuingiza kipato, Mradi ni shughuli yoyote ile ambayo inabuniwa, kupangwa na kutekelezwa kwa madhumuni ya kupata faida. Ingawaje kimsingi mradi unakuwa na wakati maalumu wa kuanza na kumalizika, kwenye shughuli za biashara mradi unaweza kuendelea kwa kipindi kirefu.

Mara nyingi tunapoanzisha shughuli za kutuingizia kipato, tunakutana na istilahi (terms) nyingi ambazo baadhi yetu tunachukulia kama ni za kawaida.

Wakati wa kupanga mradi, kuna mambo kadhaa ya kuzingatia, ambayo ni pamoja na:

  1. Gharama na matarajio ya mapato ya shughuli husika.
  2. Kuwepo kwa utaratibu wa utekelezaji; yaani namna shughuli itakavyoendeshwa.
  3. Namna shughuli zitakavyosimamiwa.
  4. Kufuatilia matakwa ya kiusimamizi, kisheria, kanuni na miongozo kuhusiana na shughuli hiyo.
  5. Kufuata masharti ya leseni husika.
  6. Utaratibu wa kufanya shughuli husika iwe endelevu.

Maandalizi ya Awali

Mradi wowote ule lazima uandaliwe. Usikirupuke tu kuanzisha mradi kwa kuwa umeona watu wengine wakifanya shughuli hiyo; au kwa kuwa una pesa au raslimali ambazo unataka kuziwekeza. Maandalizi yanahitaji ubunifu, kukusanya takwimu kuhusu soko – sasa na baadae na kufungamanisha (aligning) matarajio na hali halisi ya uchumi.

Wakati wa kubuni mradi, ni vyema kuzingatia mambo haya:

  1. Soko: Je, kutakuwa na soko la hiyo shughuli unayoanzisha?
  2. Mtaji wa kuanzisha: Hii ni pamoja na raslimali muhimu
  3. Ujuzi wa kuendesha mradi: Ni vyema kubuni mradi ambao ama anayebuni mradi ana ujuzi na uelewa wa shuvhuli inayokusudiwa au anatarajia kuwa na wataalamu watakaouendesha ili uwe endelevu.
  4. Mahali pa kufanyia shughuli hiyo: Hili litategemea aina ya shughuli inayokusudiwa.
  5. Muda wa kuanza mradi. Kwa mfano mradi wa shule ya msingi au chekechea uzingatie mihula ya kuanza masomo.

Hatua za Maandalizi ya Mradi

Kama tulivyosema awali, mradi usianzishe kwa kukurupuka au kuiga. Maandalizi ya mradi yana hatua mbalimbali, tangu kupata mwanga au wazo la kuanzisha mradi mpaka utekelezaji wake. Hatua hizi ni:

  1. Wazo au mwanga wa kuanzisha mradi.
  2. Mandalizi ya awali
  3. Uchambuzi wa aina ya shughuli inayokusudiwa.
  4. Uchambuzi wa kiuchumi na fedha
  5. Mategemeo ya mradi.

(itaendelea)

CategoryVidokezo
Write a comment:

*

Your email address will not be published.