Tutakuwa tunawaletea vidokezo muhimu kuhusu masuala ambayo mtu anatakiwa kuyazingatia anapotaka kuanza shughuli za kumuingizia kipato, kwa njia ya kutoa huduma au kuuza bidhaa. Pamoja na kusajili shughuli ya binafsi inayokuingizia kipato kama kampuni yenye dhima ya kikomo (limited liability company), unaweza pia kuisajili kama shughuli yenye umilki wa ubia (partnership) au umiliki wa pekee (sole proprietorship).

 

  1. Kuna urahisi katika kusajili majina ya biashara na shughuli zenye umilki wa ubia (partnership) au umilki wa pekee (sole proprietorship). Ubia maana yake ni shughuli ya watu zaidi ya mmoja. Umilki wa pekee ni pale mtu mmoja anaposajili na kuendesha biashara.
  2. Umilki wa pekee unamuunganisha mmilki na shughuli anayofanya, na ni njia inayopendelewa na watu wengi wenye biashara ndogo, kwani unamuunganisha mmilki na kampuni husika. Aidha, biashara binafsi zinaweza kuunganishwa kwenye jina la mwenye cheti cha namba ya utambulisho wa mlipa kodi, yaani TIN, kinachotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
  3. Matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano yamewezesha usajili wa kampuni Tanzania kufanyika mtandaoni kupitia mfumo wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).  Muda wa kusajili ni mfupi zaidi na hakuna masharti ya kuwasilisha nyaraka nyingi za kisheria.
  4. Ili kusajili kampuni ya binafsi au ubia, mfanyabiashara anakiwa kuingia kwenye tovuti ya BRELA na kujisajili. Maelezo yanapatikana https://ors.brela.go.tz/ors/start).
  5. Unapoingia kwenye mtandao huo unapatiwa namba ya kumbukumbu ili kuweza kuendelea na usajili iwapo hujakamilisha na pia kwa rejea ya taarifa zako. Ni muhimu kutumia nywila imara lakini rahisi kukumbuka.
  6. Kuna kipengele cha kujaza fomu mtandaoni; na baada ya hapo unatakiwa kuichapa, kuiweka saini, kuinakili na kuituma kama kiambatanisho.
  7. Wakati wa kujaza fomu, utatakiwa kuwasilisha Namba ya kitambulisho cha taifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na TIN.
  8. Jumla ya ada ni shilingi 20,000/=, ambamo 15,000 niada ya maombi 5,000 ni ada ya kuhifadhi nyaraka.
  9. BRELA watakutumia namba ya kumbukumbu ya malipo, na unaweza kulipia kwa huduma ya pesa kupitia simu ya mkononi au benki.
  10. Iwapo kutakuwa na ulazima, BRELA watakujulisha kuwasilisha nyaraka za ziada.
  11. Iwapo utakamilisha maombi yako kwa ufasaha, cheti cha usajili wa kampuni kitatumwa kwako baada ya muda mfupi.

Hatua zinazofuata baada ya kupata usajili ni maombi ya leseni, kulipa kodi stahiki TRA na kuanza shughuli.

Leseni nyingi za biashara, hasa za wajasiriamali wadogo zinatolewa na Halmashauri chini ya mfumo wa Serikali za Mitaa. Utatakiwa kuambatanisha fomu ya maombi ya biashara na kukidhi masharti ya kila kipengele cha biashara na cheti cha usajili wa BRELA kilichopatikana kwa utaratibu ulioainishwa mapema.

Utatakiwa kuwasilisha nyaraka za eneo unapofanyia biashara. Iwapo ni jengo lako utahitajika kuonyesha nakala ya hati ya umiliki wa ardhi au jengo na iwapo umepanga utatakiwa nakala ya mkataba wa pango, ukiwa umelipiwa ada za TRA.

Utatakiwa kulipia leseni kabla ya kupewa.

(Katika toleo lijalo tutaainisha masuala yanayohusu maombi ya leseni ambazo zina masharti yanayohitaji nyaraka kutoka taasisi nyingine. Mifano ni zile zinazohitaji vibali vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au ofisi za afya na mazingira.)

Kama una maswali, michango au taarifa za shughuli yoyote ya kibiashara, tafadhali wasilisha kupitia. tcrasaccos@go.tz

CategoryVidokezo
Write a comment:

*

Your email address will not be published.