TCRA SACCOS: Ilikotoka, ilipo na inakokwenda

  1. Utangulizi

Kihistoria vyama vya Kuweka na Kukopa (Savings and Credit Cooperative Organizations) kwa kifupi (SACCOS) vilianza rasmi mwaka 1995 na tangu hapo vimeendelea kukua na kuongezeka kitaifa na kimataifa.

Kwa muda wote tangu kuanzishwa kwake SACCOS zimeonekana kama chombo cha  kuondoa umaskini. Kutokana na mafanikio yake  hapa Tanzania Sera ya Taifa ya  National Microfinance yaani  “The National Microfinance Policy” ilipitishwa na ilipofika mwaka 2001 sera hiyo ilitekelezwa kikamilifu na tangu hapo hata mabenki ya biashara nayo yakaanza kuona SACCOS kama mteja  wao muhimu ambaye wangepaswa kushirikiana naye katika kutoa huduma za mikopo midogomidogo.

  1. Kuanzishwa kwa MKM

Historia ya TCRA SACCOS inaanza tarehe 21/4/2006 pale watumishi wa TCRA walipoanzisha Umoja wa Kusaidiana Mamlaka ya Mawasiliano kwa kifupi MKM ambao mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa Mhandisi James M. Kilaba. Malengo ya MKM pamoja na mambo mengingine ilikuwa ni kukusanya nguvu za kifedha  miongoni mwa wanachama wake ili kushirikiana  katika matatizo mbalimbali kama vile misiba, magonjwa na majanga mbalimbali.Kutokana na MKM kufanya vizuri, ikaonekana haja ya kupiga hatua moja zaidi yaani kuanzisha chombo ambacho kingewasaidia wanachama wake kujiletea maendeleo.

  1. Kuanzishwa kwa TCRA SACCOS

Tarehe 8/11/2008, takriban miaka miwili tangu kuanzishwa kwake MKM ilifanya mkutano wake Mkuu wa mwaka katika Club ya Jolly  ya Upanga Dar es salaam. Katika Mkutano huo wajumbe  kwa kauli moja waliazimia kuunda chombo cha kiuchumi zaidi amabacho kingewasaidia wanachama wake kupata mikopo ya maendeleo kwa urahisi zaidi. Hivyo katika mkutano huo MKM ilianzisha mchakato wa kuanzisha SACCOS kwa kuchagua  viongozi waanzilishi chini ya Mwenyekiti Ndugu Richard Kayombo akisaidiwa na Connie Francis, Abdul M. Hussein, MassaiJ.M Massai na Mhandisi James M. Kilaba. MKM haikuishia hapo bali ilitoa fedha  kiasi cha shs. 4,187,000.00 ili kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa.

Mchakato wa kuanzisha TCRA SACCOS ulichukua takribani miaka mitatu hadi kupata usajili 5/4/2012. Kusajiliwa kwa TCRA SACCOS kulifungua milango ya kufanyika Mkutano Mkuu wa kwanza kwa Mujibu wa Masharti na Sheria za ushirika tarehe 20/4/2012 ambapo uongozi mpya ulichaguliwa. Viongozi wa waanzilishi wa TCRA SACCOS walikuwa Ndugu Erasmo A. Mbilinyi-Mwenyekiti,  Ndugu Richard Kayombo-Makamu Mwenyekiti, na wajumbe walikuwa ni  Ndugu Abel John, Ndugu Abdul M. Hussein, Ndugu Massai J.M Massai, Ndugu Doris Saivoiye na Ndugu Benjamin Mwandete. Wajumbe wa kamati ya usimamizi waliochaguliwa walikuwa Ndugu Francis Mayila, Ndugu Conne Francis na Dk. Raynold Mfungahema.

Mkutano Mkuu wa 2 wa TCRA SACCOS ulifanyika mwaka 2013 ambapo pamoja na mambo mengine ulichagua viongozi wawili  kuziba nafasi zilizoachwa wazi na a viongozi waliondoka kwa sababu tofauti. Katika uchaguzi huo  Ndugu  Boniface L. Shoo aliteuliwa kushika nafasi ya Makamu wa  Mwenyekiti kuziba nafasi  iliyoachwa na Ndugu Richard Kayombo aliyeenda kufanya kazi katika taasisi nyingine na  Ndugu Charles Thomas alichaguliwa kujaza nafasi ya mjumbe Ndugu Abel John aliyekwenda masomoni.

Sheria mpya ya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013  iliyoanza kutumika tarehe 1/1/2014 ilisababisha  Mrajis wa Ushirika nchini kutoa waraka Na. 2 wa tarehe 6/6/2014 ambapo aliagiza vyama vyote vya Ushirika kufanya uchaguzi wa viongozi upya. Hivyo TCRA SACCOS katika mkutano wake Mkuu wa tatu uliofanyika tarehe 7/11/2015 ilifanya uchaguzi ambapo  Ndugu Erasmo A. Mbilinyi alichaguliwa tena kuendelea kuongoza chama kama mwenyekiti, Ndugu Mabel Masasi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na wajumbe waliochaguliwa ni  Ndugu Abdul M. Hussein,Ndugu Massai J.M  Massai, Ndugu Charles Thomas, Ndugu Benjamin Mwandete na  Ndugu Gabriel Mruma. Aidha ndugu Francis Mayila,Ndugu Connie Francis na Dk Raynold Mfungahema walichaguliwa kuendelea kuwa wajumbe wa Kamati ya Usimamizi.

4   Madhumuni  ya TCRA SACCOS

Kwa mujibu wa  Masharti (katiba) ya TCRA SACCOS madhumuni makuu ya TCRA SACCOS ni kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya maisha ya wanachama ili waweze kukidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii na uchumi kwa kufuata masharti ya Chama, misingi na sheria ya vyama vya ushirika.

Ili kutimiza madhumuni haya TCRA SACCOS ililazimika kutafuta vyanzo vya mapato  vyenye riba nafuu ili kuweza  kuanza kukopesha wanachama wake haraka iwezekanavyo. Katika jitihada hizo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano aliweza kuidhinisha mkopo wa masharti nafuu kwa TCRA SACCOS kufuatia maombi iliyopeleka. Mkopo huo uliiwezesha TCRA SACCOS kuanza kutoa mikopo kwa wanachama wake mwezi Machi 2014.

5   Mafanikio

Takwimu zinaonyesha kuwa chama kinaendelea kukua katika nyanja mbalimbali. Kwa upande wa wanachama, wameongezeka kutoka 109 mwaka 2013 hadi 219 Julai 2021. Pia Akiba za Wanachama ziliongezeka kutoka TZS 622,920,400 mwaka 2015 hadi TZS 2,748,142,683 Julai 2021. Hisa kutoka TZS 34,500,000 mwaka 2015 hadi TZS 1,180,049,910 Julai 2021, na Amana kutoka TZS 6,200,000 mwaka 2015 hadi TZS 70,299,200 Julai 2021. Aidha katika kipindi cha miaka saba (2014-2021, Chama kiliweza kutoa mikopo yenye thamani ya TZS 11,127,850,000.00.

Hali kadhalika chama kiliweza kuajiri meneja wake wa kwanza ndugu Damas Mapunda ambaye alisaidia  kusimamia ukaguzi wa hesabu na na hivyo chama  kupata hati safi  mara tatu mfululizo. Katika kipindi hicho  chama kilinunua vitendea kazi mbali mbali kama vile kompyuta, mashine ya kudurufu karatasi na skana pamoja na software ya kutunza kumbukumbu za fedha za chama na wanachama. Hivi sasa chama  kimeanzisha Tovuti ambayo pia ina huduma za papo kwa pao (Online Services) na hivyo kukifanya kuwa miongoni mwa vyama vichache vinavyofanya kazi zake zake kisasa kabisa.

6   Malengo ya muda mfupi na mrefu

TCRA SACCOS imejiwekea malengo ya muda mfupi na mrefu kama yalivyoainishwa katika Mpango Mkakati wa  Mwaka 2016-20 ambapo imedhamiria kufanya yafuatayo:-

  1. Kuendelea kuongeza idadi ya wanachama kufikia 200 kutoka idadi ya sasa ya 128 ifikapo mwaka 2020;
  2. Kuendelea kutoa mafunzo kwa wanachama ili kukuza uelewa  kuhusu chughuli za SACCOS na ujasiriamali;
  3. Kuongeza huduma zitolewazo na TCRA SACCOS kutoka asilimia 60 ya sasa hadi asilimia 100 ifikao 2020;
  4. Kuongeza ufanisi wa shughuli zake kwa kuhakikisha matumizi yanabaki kuwa chini ya 50% ya mapato ya jumla;
  5. Kuongeza mtaji wa chama kwa 6% ya raslimali zake;
  6. Kuajiri  na kuwaendeleza watumishi waliobobea katika Ushirika;
  7. Kujenga mifumo ya kisasa ya taarifa yaani Management Information systems;
  8. Kujenga utayari wa kukabiliana na majanga.

7   Hitimisho

Chama chetu kimeanza vizuri na kinakwenda vizuri. Hii imetokana na kuungwa mkono na wanachama na wadau wengine kama ukiwepo Uongozi wa TCRA, Ofisi ya Ushirika Wilaya, vyombo vya fedha na wadau wengine. Hivyo natoa wito kwa wanachama wote na washirika wetu wengine kuendelea kutuunga mkono ili kutimiza  ndoto ya dira yetu ambayo ni kuwa chama cha Ushirika cha kifedha cha kiwango cha kimataifa na dhima yetu  ambayo ni kuborehsa ustawi wa wanachama wetu kwa kunyanyua hali zao za kiuchumi  na kijamii kwa kuwapatia huduma mbalimbali  za kifedha zenye ubora wa hali ya juu.

Ushirika-Suluhisho la Mtaji!

SACCOS- Pamoja tujenge Uchumi!