Ndugu Wanachama,

Kwa mujibu wa Katiba ya TCRA SACCOS Ltd, madhumuni makuu ya Chama ni kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya maisha ya wanachama ili waweze kukidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii na uchumi kwa kufuata masharti ya Chama, kwa kuzingatia misingi na sheria ya vyama vya ushirika. Ili kutimiza madhumuni haya TCRA SACCOS Ltd ililazimika kutafuta vyanzo vya mapato vyenye riba nafuu ili kuweza kuanza kukopesha wanachama wake kwa haraka iwezekanavyo. Katika jitihada hizo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano aliweza kuidhinisha mkopo wa TAS 500,000,000 wenye masharti nafuu kwa TCRA SACCOS Ltd kufuatia maombi yaliyopelekwa kwake. Mkopo huo uliiwezesha TCRA SACCOS Ltd kuanza kutoa mikopo kwa wanachama wake kuanzia mwezi Machi 2014. Aidha Chama kimeendelea kuulipa mkopo huu kwa riba nafuu na sasa ninafurahi kuwataarifu Wanachama kuwa deni hadi kufikia Disemba 2023 deni litakalobaki ni TAS 49,400,000.

Kuanzishwa kwa MKM

Historia ya TCRA SACCOS inaanza tarehe 21/4/2006 pale watumishi wa TCRA walipoanzisha Umoja wa Kusaidiana Mamlaka ya Mawasiliano kwa kifupi MKM ambao mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa Mhandisi James M. Kilaba. Malengo ya MKM pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kukusanya nguvu za kifedha miongoni mwa wanachama wake ili kushirikiana katika matatizo mbalimbali kama vile misiba, magonjwa na majanga mbalimbali. Kutokana na MKM kufanya vizuri, ikaonekana kuna haja ya kupiga hatua moja zaidi yaani kuanzisha chombo ambacho kingewasaidia wanachama wake kujiletea maendeleo.

Kuanzishwa kwa TCRA SACCOS LTD

Tarehe 8/11/2008, takribani miaka miwili tangu kuanzishwa kwake MKM ilifanya mkutano wake Mkuu wa mwaka katika Club ya Jolly ya Upanga Dar es salaam. Katika Mkutano huo wajumbe kwa kauli moja waliazimia kuunda chombo cha kiuchumi zaidi ambacho kingewasaidia wanachama wake kupata mikopo ya maendeleo kwa urahisi zaidi. Hivyo katika mkutano huo MKM ilianzisha mchakato wa kuanzisha SACCOS kwa kuchagua viongozi waanzilishi chini ya Mwenyekiti Ndugu Richard Kayombo akisaidiwa na Ms Connie Francis, Abdul Muhidin Hussein na Massai John Massai (Marehemu). MKM ilitoa fedha kiasi cha TAS. 4,187,000 ili kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa.

Mchakato wa kuanzisha TCRA SACCOS ulichukua takriban miaka mitatu hadi kupata usajili 5/4/2011 kwa namba ya usajili DSR.1314. Kusajiliwa kwa TCRA SACCOS Ltd kulifungua milango ya kufanyika Mkutano Mkuu wa kwanza kwa Mujibu wa Masharti na Sheria za Ushirika tarehe 20/4/2012 ambapo uongozi mpya ulichaguliwa. Viongozi waanzilishi wa TCRA SACCOS Ltd walikuwa Ndugu Erasmo Anthony Mbilinyi-Mwenyekiti, Ndugu Richard Kayombo-Makamu Mwenyekiti, na wajumbe walikuwa ni Ndugu Abel John, Ndugu Abdul M. Hussein, Ndugu Massai J.M Massai, Ndugu Doris Saivoiye na Ndugu Benjamin Mwandete. Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi waliochaguliwa walikuwa Ndugu Francis Mayila, Ndugu Connie Francis na Dk. Raynold Mfungahema.

SALAMU KUTOKA MWENYEKITI WA BODI KWA WANACHAMA

Ndugu Wanachama,

Chama chetu cha Ushirika cha TCRA SACCOS Ltd kilipata usajili wa kudumu kuwa SACCOS tarehe 05/04/2011 na kupata hati Na.DSR 1314, Mafanikio haya ya kupata usajili hayawezi kupita bila kuwataja viongozi waliokuwa chini ya Mwenyekiti Ndugu Richard Kayombo,Viongozi hao ni Ms.Connie Francis, Ndugu Massai John Massai na Ndugu Abdul Muhidin Hussein.

Sheria mpya ya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013 iliyoanza kutumika tarehe 01/01/2014 ilileta mabadiliko ambayo Mrajis wa Ushirika nchini alitoa waraka Na. 2 wa tarehe 6/6/2014 ambapo aliagiza vyama vyote vya Ushirika kufanya uchaguzi wa viongozi upya.

Hivyo TCRA SACCOS Ltd katika mkutano wake Mkuu wa tatu uliofanyika tarehe 7/11/2015 ilifanya uchaguzi ambapo Ndugu Erasmo A. Mbilinyi alichaguliwa kuongoza Chama kama Mwenyekiti, Ndugu Mabel Masasi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na wajumbe waliochaguliwa ni Ndugu Abdul M. Hussein, Ndugu Massai J.M Massai(Marehemu), Ndugu Charles Thomas, Ndugu Benjamin Mwandete na Ndugu Gabriel Mruma. Aidha ndugu Francis Mayila, Ndugu Connie Francis na Dk. Raynold Mfungahema walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Usimamizi.

Viongozi waliopo sasa madarakani walichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika tarehe 13/11/2020 ambapo Ndugu Thadayo Joseph Ringo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, ndugu Batholomew M. Waranse kuwa Makamu Mwenyekiti na wajumbe ni Ndugu Beatrice Lema, ndugu Amina Ramadhani, ndugu Mwesigwa Felician, ndugu Abdulrahman Issa Millas na ndugu Abel John. Kamati ya Usimamizi ni ndugu Napalite Magingo,ndugu Patrice L. Mapunda na ndugu Kelvin Massawe. Viongozi hawa wanamaliza muhula wao wa uongozi mwaka huu 2023.

AKIBA YA SACCOS

Akiba za Wanachama ziliongezeka kutoka TAS 2,637,140,416 Mwaka 2020 hadi TAS 3,715,091,689 ilipofika tarehe 31 Oktoba 2023.

HISA ZA SACCOS

Hisa za wananchama zilipungua kutoka TAS 1,427,925,750 Mwaka 2020 hadi TAS 681,110,000 ilipofika tarehe 31 Oktoba 2023.

Taarifa za Hisa

Chama kinapitia kipindi ambacho Hisa za Wanachama kwa miaka mitatu zimeshuka kutoka TAS 1,427,925,750.00 hadi TAS 681,110,000.00 hii ni kutokana na sababu zifuatazo;

  • Chama kutotoa gawio kutokana sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika wa kuweka na kukopa ambapo kama uwiano wa Mtaji Taasisi (Institutional Capital) uko chini ya 6% Chama hakiwezi kutoa gawio isipokuwa kwa idhini ya Mraji;
  • Baadhi ya Wanachama waliokuwa wamewekeza kiwango kikubwa cha hisa ndani ya Chama walistaafu na kuondoka katika Chama;
  • Baadhi ya wanachama kuhama taasisi na kwenda taasisi nyingine na hivyo kujitoa uanachama;
  • Baadhi ya Wanachama waliostaafu na kuhamia taasisi nyingine kutumia Hisa kulipa madeni yao;
  • WanachAma kupendelea kuweka zaidi fedha zao kwenye Amana na Akiba na sio kwenye Hisa.

MALI ZA SACCOS

Mali zote za Chama (Total Assets) zimeongezeka kutoka TAS 4,403,289,907 Mwaka 2020 hadi TAS 5,441,048,862 ilipofika tarehe 31 Oktoba 2023.

MTAJI WA SACCOS

Mtaji wa Chama uliongezeka kutoka TAS 347,965,648 Mwaka 2020 hadi TAS 704,650,049 ilipofika tarehe 31 Oktoba 2023.

AMANA ZA SACCOS

Amana ziliongezeka kutoka TAS. 90,272,517 Mwaka 2020 hadi TAS 258,989,842 ilipofika tarehe 31 Oktoba 2023.

MIKOPO YA SACCOS

Mikopo imeongezeka kutoka TAS 3,013,969,132 mwaka 2020 hadi TAS 4,728,674,265 mwaka 2023 (outstanding loans).

Matumizi ya Teknolojia Katika Uendeshaji wa Chama

Chama kiliamua kutumia teknolojia tangu siku ya kwanza ambapo mahesabu yote ya Chama yaliingia kwenye mfumo wa Komputa kupitia software ya Foresight Solution, mfumo ambao umesaidia kuhakikisha mahesabu ya Chama yanakuwa sahihi na taarifa mbali mbali zinatolewa kwa usahihi na kwa wakati. Aidha Chama kina vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi kama vile computer, Projector, Printers na Binder Machine. Pia mifumo ya TEHAMA ya TCRA imekisaidia sana Chama katika masuala ya utunzaji wa taarifa wa ziada (Back Up) kupitia recovery site zake ili kuhakikisha taarifa za Wanachama zinabaki salama endapo yatatokea majanga.

Aidha Chama kina Tovuti yake (www.tcrasaccos.co.tz) ambayo matukio yote muhimu ya Chama na taarifa mbalimbali huwekwa humo. Mfano wa taarifa ni pamoja na Semina mbalimbali kwa Wanachama, mikutano ya Wanachama, namna ya kuandaa mpango biashara, na mbinu mbalimbali za uuzaji bidhaa kupitia mitandao ya kijamii. Kwa taarifa zaidi tunashauri Wanachama kutembelea tovuti yao ya Chama kwa lengo la kupata taarifa, kujifunza na kutoa michango ya kuiboresha.

Aidha Chama kipo kwenye harakati za kuiboresha zaidi tovuti hii ili iwe ya kisasa zaidi na manufaa kwa Wanachama. Pamoja na maboresho hayo, Chama kwenye mpango kazi wa muda mrefu kimeweka nia ya kujenga na kuendesha mfumo wake wenyewe wa kuchakata taarida za Wanachama, kutoa huduma mbalimbali (ikiwa pamoja na utoaji mikopo kwa njia ya kidijiti), pamoja na kuutumia mfumo huo kama sehemu ya kupata kipato kwa kuwezesha vyama vingine vya ushirika kuutumia na kwa malipo yatakayoongeza kipato cha Chama.

Hati Safi za Ukaguzi

Katika kipindi chote cha miaka mitatu ya Bodi hii Chama kimeweza kupata Hati Safi kila ukaguzi. Pongezi kwa Watendaji kwa kupokea maelekezo kutoka kwa Bodi na kuyafanyia kazi na kwa wajumbe wa Bodi kwa kusimamia shughuli za Chama kwa umakini.

Ushirikiano na Uongozi wa TCRA

Chama kinajivunia uhusiano thabiti baina yake na uongozi wa TCRA, ambao licha ya kutoa mtaji wa kuanzia kukopesha wanachama, umetoa misaada mingine mbali mbali kama vile chumba cha ofisi, malipo ya umeme, maji, samani za ofisi na ukumbi wa mikutano kwa mikutano yote iliyofanyika hadi sasa. Aidha TCRA imeendelea kutusaidia katika kukusanya malipo ya marejesho ya mikopo kutoka kwenye mishahara ya Wanachacma waliowengi, pamoja na kututambulisha kwa waajiri wa Wanachama waliohamia taasisi.

Ushirikiano Kutoka Tume ya Ushiriki na Ofisi ya Ushirika ya Manispaa ya Ubungo

Chama kinapata ushirikiano mkubwa kutoka Ofisi ya Ushirika Manispaa ya Ubungo kupitia ushauri na ukaguzi kabla wakaguzi wa nje hawajafika. Aidha Chama kinapata ushirikiano wa kutosha kutoka ofisi ya Mrajisi wa vya Vyama vya Ushirika kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Ushuhuda wa Wanachama walionufaika na Mikopo kutoka TCRA SACCOS

Chama kimetoa mikopo mbalimbali ambayo imewanufaisha Wanachama. Na baadhi ya Wanachama wameweza kujenga shule, kuanzisha viwanda, kufungua mashamba makubwa, kutengeneza “green house” n.k.

Uwekezaji katika Benki ya Ushirika ya KCBL

Chama kimeweza kuwekeza kianzio katika Benki ya Ushirika. Idadi ya hisa 4000 zimenunuliwa kwa thamani ya TAS 2,000,000 na kuwekezwa katika benki hiyo tarajiwa ya Ushirika.

Utoaji wa Gawio na Faida kwa Wanachama

Kwa kipindi cha miaka mitatu mwaka 2021 Chama kilitoa gawio la TAS 100,893,563. Baada ya kuona kuwa Mtaji Taasisi umeshuka na itakuwa vigumu kutoa gawio, Bodi uliangalia njia mbadala ya kuhakikisha Wanachama wanaendelea kunufaika na uwekezaji wao ndani ya Chama hivyo mwaka huo huo 2021 Chama kilitoa riba ya TAS 127,122,233.00 na mwaka 2022 kilitoa faida kwa Wanachama TAS 113,230,398.00 kwenye Akiba, Hisa na Amana na kwa mwaka 2023 Chama kimetenga jumla ya TAS 190,000,000.00 kwa ajili ya kutoa faida kwa Wanachama. Hivyo kwa miaka yote mitatu Chama kimetoa jumla ya TAS 531,336,194.00 kwenda kwa Wanachama.
Chama kilianza kutoa gawio kwa wanachama mwaka 2017 ambapo mwaka huo TAS 17,390,000.00 walilipwa wanachama kama gawio, mwaka 2018 TAS 56,313,000.00, mwaka 2019 TAS 62,601,000.00, mwaka 2020 TAS 70,105,222.00 jumla ya magawio yote kwa miaka minne ilikuwa ni TAS 206,409,222 ambazo zilikwenda kwa Wanachama.
Tangu kuanza kutolewa kwa gawio na faida kwa Wanachama kwa kipindi cha miaka minane (8), Bodi inayomaliza muda wake iliweza kusimamia Chama, na hivyo kuwezesha Wanachama kupata faida na gawio kwa kiasi cha 72% cha fedha zote zilizotolewa kama faida na gawio la Wanachama toka kuanzishwa kwa Chama.

Usajili Mpya wa Chama

Katika kipindi cha miaka mitatu Chama kilifanikiwa kusajiliwa kuwa SACCOS daraja B namba ya usajili MSP3-TCDC/2021/0044. Sifa ya kuwa SACCOS daraja B ni kuwa na mtaji unaozidi TAS 200,000,000.

Kuongezeka Huduma Mbalimbali Zaidi ya Utoaji

Kwa kipindi cha miaka mitatu Chama kimeweza kuongeza huduma nyingine zaidi ya utoaji mikopo. Huduma hizo ni uwakala wa makampuni ya simu (Tigo Pesa, na M-pesa), wakala wa benki ya CRDB na wakala wa Bima ambapo Chama kinahudumia Wanachama kukata bima mbali mbali ikiwa ni pamoja na zile za vyombo vyao vya usafiri.

MWISHO

Katika kuhitimisha mhula huu wa uongozi katika Chama, ni Dhahiri kuwa tumekitumikia Chama chetu kwa bidi kwa kadri tulivyojaliwa, Chama kina “AFYA” na “NGUVU”. Ni imani yangu kuwa Uongozi utakaoendeleza Chama utaendeleza fikra njema na “UBUNIFU” zaidi ili kukipeleka juu zaidi kwa mafanikio.

Ninawaomba Wanachama wenzangu tuchague Viongozi wetu kwa kuzingatia weledi, uadilifu na wenye maarifa ya kukiongoza Chama chetu. Hawa ni Viongozi watakaoendeleza vizuri Chama chetu katika siku zijazo na kuinua uchumi wetu.

Kwa maelezo haya, niwashukuru tena Wanachama wote kwa kuniamini kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa kipindi cha miaka mitatu. Niwashukuru Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Chama kwa kunisaidia katika uongozi wangu. Aidha, niwashukuru Viongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuendelea kukiunga mkono Chama chetu. Kipekee na kwa dhati kabisa, naomba kuwashukuru sana Watendaji wa Chama kwa kuratibu shughuli zote za Chama kwa kipindi nilichokuwa Mwenyekiti, kwa kweli wamekuwa na msaada mkubwa sana kwangu binafsi, katika kutoa ushauri kwenye maamuzi tuliyoyafikia kama Bodi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia vyama vya ushirika.

Kwa niaba ya Bodi nzima ya Chama inayomaliza muda wake, na mimi binafsi, ninawaomba radhi sana pale ambapo tuliwakosea, pale tulipofanya kwa ulegevu na pale ambapo hatukufanya vizuri.

Ninawaomba tuwape ushirikiano viongozi watakao chaguliwa ili kwa pamoja tuendelee kuijenga TCRA SACCOS LTD kwenda kwenye viwango vingine (to the next higher level).

Kwenu nyote, nasema Asanteni sana, na MUNGU Awabariki sana!

Pamoja na salamu za Ushirika

Thadayo Joseph Jonas Ringo

Mwenyekiti, TCRA SACCOS LTD